
New York, Marekani
Miaka 30 iliyopita, hofu ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi ikiwa juu, nyota wa mpira wa kikapu wa Ligi ya NBA ya Marekani, Magic Johnson alitangaza kuwa ni muathirika wa Virusi vya Ukimwi (VVU).
Johnson ambaye baada ya kutangaza kuathirika na VVU pia alitangaza kustaafu mpira wa kikapu akiwa ndio kwanza ana miaka 32, anabaki kuwa miongoni mwa mastaa wa kikapu duniani waliojipatia umaarufu na utajiri kupitia mchezo huo akishinda karibu kila kitu.
Hadi sasa Ukimwi hauna dawa, faraja iliyopo ni vidonge vya kufubaza virusi hivyo, maana yake ni kwamba hofu juu ya ugonjwa huo bado ipo ingawa si kama ilivyokuwa miaka 30 iliyopita.
Kwa maana nyingine hatua ya Johnson kutangaza kwamba ana VVU kwa wakati huo ilihitaji ujasiri wa aina yake hasa kwa uzoefu wa nchi za Afrika, wakati huo Ukimwi ulihusishwa na laana na majanga mengine, unyanyapaa ulikuwa juu, baadhi ya waathirika walifichwa ndani.

Katika kipindi hicho pia ilijengeka dhana kwamba mgonjwa wa Ukimwi anasubiri siku ya kufa. Yote hayo hayakumtisha Johnson ambaye sasa ana miaka 62 na ametimiza miaka 30 tangu atangaze kuathirika na VVU
Ilikuwa ni Novemba 7, 1991, unyanyapaa na hofu juu ya Ukimwi vikiwa juu, Johnson alitangaza mbele ya waandishi wa habari kwamba vipimo vilionyesha ameathirika.
Katika taarifa yake, Johnson aliyetamba na timu ya Los Angeles Lakers alisema kwamba mkewe, Cookie ambaye alikuwa mjamzito hakuwa na maambukizi na tangu hapo akatangaza kujitolea katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
Ni miaka 30 yaani miongo mitatu sasa imepita tangu Johnson auvae ujasiri wa kutangaza kuathirika na VVU lakini ajabu ni kwamba bado ni Johnson yule yule, tabasamu lake lile lile kama vile hajaathiriwa na maradhi ambayo kwa wengi huja na hofu ya kifo.
Katika kutangaza kwake kuathirika na VVU Johnson alisema kuwa hajui aliupataje ugonjwa huo ingawa aliuhusisha na tabia yke ya kuwa na wapenzi wengi katika maisha ya ustaa wa kikapu.
Ni hivi karibuni chanzo kimoja cha habari za mpira wa kikapu nchini Marekani kiliandika katika moja ya taarifa zake kwamba kwa mwaka Johnson wakati huo akiwa staa aliweza kuwa na mahusiano na wanawake zaidi ya 100.
Hata hivyo kauli ya Johnson kujitangaza kuwa ana VVU pamoja na kwamba ilishangaza na kushtua wengi pia haikuachwa ipite hivi hivi bila ya kutiliwa shaka.
Wako waliodai kwamba Johnson hakuwa na VVU bali uamuzi wake wa kujitangaza hadharani ilikuwa ni mkakati wa kuwatetea wanaofanya mapenzi kinyume na maumbile ambao wakati huo ndio waliohusishwa zaidi na maradhi hayo.
Pia wako waliodai kwamba Johnson kujitangaza kuathirika na VVU ilikuwa kama njia mojawapo ya kuwaamsha waliokuwa wakiihusisha ugonjwa huo ni watu wanaofanya mapenzi kinyume na maumbile badala yake alitaka watu wajue kwamba kila mtu yuko katika hatari ya kuambukizwa maradhi hayo.
Ukiachana na waliotilia shaka kuathirika kwa Johnson, uamuzi wake wa kujitangaza hadharani ulimpa umaarufu, aliwahi kupongezwa na aliyekuwa Rais wa Marekani, George Bush ambaye alisema Magic ni shujaa kwa mtu yeyote mpenda michezo.
Zaidi ya hilo amekuwa akialikwa katika matukio mbali mbali ya kimataifa akitumiwa kama shujaa ambaye anahamasisha watu kutowanyanyapaa wagonjwa wa Ukimwi na kuwafanya waishi kwa matumaini.